Uharamu wa Ulevi..
Ulevi ni mojawapo ya dhambi katika madhambi makubwa sabini, madhara yake ni makubwa kwa mtu binafsi na jamii nzima. Mwenyezi Mungu S.W.T. ameuharamisha ulevi na vile vitendo vyote vinavyohusiana navyo kama vile: Kuukamua, kuupika, kuubeba, kuuza na kumpa mtu zawadi. 
Ulevi ni moja ya njia kubwa ambayo Shetani anaitumia kuwapoteza watu, na mtu akishaingia katika mtego huo basi anamfunga kwa kamba yake madhubuti asiweze kutoka mpaka inamuangamiza yule mnywaji na kumpeleka katika matokeo ya hatari na mabaya. Ulevi unamtoa akili mlevi anapounywa na mara anapotokwa na akili hufanya mambo ambayo humuangamiza mlevi mwenyewe; ikiwa ni pamoja na kufanya maasi makubwa yanayomstahikia adhabu kali ya Mwenyezi Mungu, na athari yake inawagusa watu wengine katika jamii. Mwenyezi Mungu S.W.T. kasema katika Quran Kwenye Suratil Maida aya ya 90 mpaka 91
“Enyi mlioamini! Bila shaka ulevi na kamari na kuabudiwa (kuombwa) asiyekuwa Mwenyezi Mungu, na kutazamia kwa mishale ya kupigia ramli; (yote haya) ni uchafu (ni) katika kazi ya Shetani. Basi jiepusheni navyo, ili mpate kufaulu (kutengenekewa). Hakika Shetani anataka kukutilieni uadui na bughudha baina yenu kwa ajili ya ulevi na kamari na anataka kukuzuilieni kumkumbuka Mwenyezi Mungu na (kukuzuilieni) kusali. Basi je, mtaacha (mabaya hayo)?” 
Na katika usemi wa Mtume Mohamad SWA iliyopokelewa na Sayyidna Uthmaan bin Affaan R.A.A. na kutolewa na Nnasaai, kasema
“Jiepusheni na ulevi, hakika ulevi ni mama wa mabaya (maovu).” 
Mtume Muhamad S.A.W. kutubainishia wazi kuwa ulevi ni kitu kinacholewesha na kitakavyokuwa namna yake au jina lake. Kama ilivyothibiti katika Hadithi iliyopokelewa na Ibn Umar R.A.A. na kutolewa na Muslim, Mtume Muhamad S.A.W. kasema,
“Kila kinacholewesha ni ulevi, na kila kinacholewesha ni haramu. Atakaekunywa ulevi duniani akafa hakutubu nao ataharamishiwa katika Akhera.”
MLEVI NI KAMA MTU ANAEABUDU SANAMU.
Uislamu umemfananisha mlevi aliyekufa naye hakutubu ni sawasawa na kama yule mtu ambaye kafa akiwa anaabudu sanamu. Ibn Abbaas R.A.A. kasema “Ilipoteremshwa aya ya kuharamishwa kunywa ulevi, Masahaba waliambiana kwamba ulevi umeharamishwa, kisha wakaufananisha kuunywa sawa na shirki.” Mtume Muhamad S.A.W. kasema katika Hadithi iliyopokelewa na Abu Huraira R.A.A. na kutolewa na Ahmad, “
“Mnywaji ulevi ni kama anaeabudu sanamu (mshirikina).” 
HAIJUZU KUJITIBU KWA ULEVI.
Watu wengi wanauliza, “Jee! Unaweza kujitibu kwa ulevi?” Swali hili lilijibiwa toka zama za Mtume S.A.W. alipokuwa hai kwa uthibitisho wa Hadithi iliyopokelewa na Ummu Salamah R.A.A.H. (mkewe Mtume S.A.W.) na kutolewa na Baihaqi na Abu Yaaly, kasema Ummu Salamah R.A.A.H., “Mtoto wake wa kike alikuwa mgonjwa, kwa hivyo akaloweka tende kwenye chungu. Mtume S.A.W akaingia nyumbani kwake akaona zile tende zilizolowekwa na kuchachuka zinatoa mapovu. Akauliza: “Nini hii, ewe Ummu Salamah?” Nikamwambia kwamba ninachachua tende kwa ajili ya kumtibu mtoto wangu. Mtume Muhamad S.A.W. akajibu akasema, “
“Hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu hakujaalia kupona kwa umma wangu (kwa mambo) aliyowaharamishia.”
Kwa hiyo Uislamu umeharamisha kutumia ulevi kwa ajili ya tiba, kwani ulevi ungeliruhusiwa kutumiwa kwa ajili ya tiba bila shaka ingeliwasababishia watu wengi kuunywa au kujitafutia ugonjwa wa uongo, na wangelichukulia kuwa kweli ulevi ni tiba yenye manufaa kwa ajili ya afya ya mwili.
Na mtu mmoja alimwambia Mtume Muhamad S.A.W. kwamba tunatumia pombe kwa ajili ya tiba ya maradhi, Mtume S.A.W. alimjibu akasema kama ilivyokuja katika Hadithi iliyotolewa na Ttirmidhi, “
“Hakika (huo) ulevi si dawa lakini ulevi ni ugonjwa.”
Pia imefahamika wazi katika Hadithi sahihi kwamba: Ulevi unanywewa na watu wasioamini Mwenyezi Mungu na siku ya Kiyama. Katika Hadithi iliyopokelewa na Abu Musa L-Ash`ary R.A.A. kasema, “Kilipoletwa chungu cha maji ya matunda yaliyochachuka kwa Mtume Muhamad S.A.W., Mtume Muhamad S.A.W. akasema, “
“Vunjilia mbali kwenye ukuta huu (yaani mwagilia mbali). Hakika hiki kinywaji (kinanywewa na) yule asiyeamini Mwenyezi Mungu na siku ya Mwisho (ndio tu anaekunywa).” 
Na pia imefahamika katika Hadithi mbili sahihi kwamba, “Kila kinacholewesha ni haramu, ikiwa kwa wingi au kidogo.” Sahaba Abu Musa L-`Ash`ary R.A.A. alimuuliza Mtume Muhamad S.A.W. “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Tupe hukumu kati ya vinywaji viwili. Kimoja kimetengenezwa kutokana na asali na kingine kutokana na shayiri au ngano. Kila kimoja kimechachuka.”
Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W. akajibu,
“Kila kinacholewesha ni haramu.”
Na pia akasema
“Kinacholewesha kwa wingi wake (hata) kidogo yake ni haramu.”
HASARA ZA MLEVI DUNIANI NA AKHERA.
1.MLEVI HAKUBALIWI SALA YAKE MASIKU ARUBAINI.
Mwenyezi Mungu S.W.T. hakubali Sala ya mtu mlevi kwa masiku arubaini. Ila ikiwa atatubia basi Mwenyezi Mungu S.W.T. atapokea toba yake. Lakini akirejea tena kunywa ulevi na Sala yake pia haitokubaliwa kwa masiku arubaini. Kwa hali hiyo akifa naye hakutubu basi hesabu yake huhesabiwa sawa na mtu yule asiyesali. Mtume Muhamad S.A.W. kasema katika Hadithi iliyopokelewa na Abu Dhar R.A.A. na iliyotolewa na Ahmad, kasema “
“Atakayekunywa pombe Mwenyezi Mungu hatomkubalia Sala kwa masiku arubaini. Akitubia Mwenyezi Mungu atamkubalia toba yake, lakini akirejea (kunywa ulevi) atakuwa kama vile mwanzo (kabla ya kutubu).”
2.MLEVI AKIFA BILA YA KUTUBU HAINGII PEPONI.
Mtume S.A.W. ameelezea wazi kabisa katika Hadithi sahihi ya kwamba mlevi atakaekufa bila ya kutubu haingii Peponi. Kwa hivyo ni juu ya mlevi mwenyewe kujikatia shauri, ama kujiangamiza au kujisalimisha kwa kuacha kunywa ulevi. Mtume Muhamad S.A.W. kasema katika Hadithi iliyopokelewa na Ibn `Umar R.A.A. na iliyotolewa na Nnasaai, kasema “
“Haingii Peponi asiewaheshimu wazazi na wala mnywaji ulevi.”
3.MWISLAMU ANANYANG`ANYWA IMANI YAKE WAKATI ULE WA KUUNYWA ULEVI.
Mwenyezi Mungu S.W.T. anamnyang`anya imani yake Mwislamu wakati ule anapokunywa ulevi. Kwani Uislamu umekuja kuharamisha ulevi ikiwa kunywa kidogo au kwa wingi, na haiwi kitu kizuri na kibaya kuwa pamoja kwa wakati mmoja. Mtume Muhamad S.A.W kasema katika Hadithi iliyopokelewa na Abu Huraira R.A.A. na iliyotolewa na L-Bukhari na Muslim na Imam Rabi`i, Mtume S.A.W. kasema, “
“Hazini mzinifu wakati anapozini naye ni Mwislamu, wala haibi mwizi wakati wa kuiba naye ni Muislamu, wala hanywi ulevi wakati wa kuunywa naye ni Muislamu. Lakini akitubu Mwenyezi Mungu anapokea toba yake.” 
[SIZE="4"]
5.MLEVI ANALAANIWA NA MWENYEZI MUNGU.
Binadamu lazima ajiangalie na ajiepushe ili asiipate laana ya Mwenyezi Mungu S.W.T.. Kwani laana ni kitu kibaya kabisa, kinamfanya mtu yule aliyelaaniwa kupotea katika upotofu asijue njia ya haki, na akakiona kitendo kibaya kuwa ni kizuri na kizuri kibaya. Na hata mambo yake ya duniani na Akhera hayatakuwa ya kuongoka na ya balaa za kila aina. Mtume Muhamad S.A.W. kasema katika Hadithi iliyopokelewa na Ibn Abbas R.A.A. na iliyotolewa na Ahmad, kasema “
“Alinijia (Malaika) Jibril (A.S.) akasema: Ewe Muhammad (S.A.W.)! Hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu ameulani ulevi, na mtengenezaji, na mkemaji, na anayeunywa, na mbebaji, na anayepelekewa, na muuzaji, na mnunuaji, na anayenywesha na anayenyweshwa.”
 
 
 
 
 
 
          
      
 
  
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
No comments:
Post a Comment