Ndugu zangu waislamu, zifuatazo ni maadhi ya hadithi sahihi zinazogusia picha.
Þ Imepokewa kutoka kwa Jaabir–Allah amuwiye radhi-amesema: "Mtume wa Allah–Rehema na Amani zimshukie–alikataza (kuwekwa) picha/vinyago ndani ya nyumba na akakataza kutengenezwa hilo". Tirmidhiy [1749]–Allah amrehemu.
Þ Imepokewa kutoka kwa Abdillah Ibn Masoud–Allah amuwiye radhi–amesema: Mtume wa Allah–Rehema na Amani zimshukie–amesema: "Hakika watu watakao kuwa na adhabu kali kuliko watu wote siku ya Kiyama ni wachora/wapiga picha." Muslim [2109]–Allah amrehemu.
Þ Mtume wa Allah–Rehema na Amani zimshukie–amesema: "Hakika wale wanao tengeneza picha hizi, wataadhibiwa siku ya Kiyama waambiwe: Vihuini (vipeni uhai) mlivyo viumba". Bukhari [5607] & Muslim [2108]–Allah awarehemu.
Þ Imepokewa kutoka kwa Said Ibn Abil–Hassan–amesema: Mtu mmoja alikuja kwa Ibn Abbas–Allah awawiye radhi–akasema: Hakika mimi ni mtu ninaye tengeneza hizi picha, basi hebu nipe fat-wa katika suala hili. Akasema (Ibn Abbas): Nikaribie, akamkurubia. Halafu akamwambia (mara ya pili): Nikaribie, akamkurubia mpaka akamshika kichwani kwa mkono wake, akasema: Ninakueleza nilicho kisikia kutoka kwa Mtume wa Allah–Rehema na Amani zimshukie. Nilimsikia Mtume wa Allah akisema: " Kila mtengeneza picha ataingia motoni, atafanyiwa kwa kila picha aliyo itengeneza nafsi, basi imuadhibu ndani ya Jahanamu". Na akasema: Ikiwa ni lazima utengeneze (kwa kuwa ndio chumo lako), basi tengeneza (picha /sanamu ya) mti, na kile kisicho na nafsi (roho)". Bukhaariy & Muslim–Allah awawiye radhi.
Þ Na imepokewa kutoka kwa Abu Twalhah–Allah amuwiye radhi–kwamba yeye amesema: Hakika Mtume wa Allah–Rehema na Amani zimshukie–amesema: "Hakika malaika hawaingii ndani ya nyumba ambayo mna ndani yake mbwa wala sura/picha za masanamu". Bukhaariy [3053] & Muslim [2106]–Allah awarehemu.

No comments:
Post a Comment