Friday, April 20, 2012

Ukabila, uzawa sumu ya udugu wa Kiislamu


UKABILA, utaifa, uzawa ni maneno yaliyozoeleka sana masikioni mwa watu. 
Imefikia hatua ambayo hauangaliwi ufanisi wa kazi inayohitajika au kufanyika bali yanatazamwa haya maeneo matatu kwanza kama yanakubalika kulingana na nafasi yenyewe.

KWA mtazamo wa Uislamu maneno haya matatu hayana nafasi kabisa badala yake uangaliwa ufanisi tu. Bila kujali huyo muhusika ni kutoka kabila lipi au taifa gani wala alipozaliwa.
Uislamu kama mfumo kamili wa maisha umemuweka mwanaadamu katika nafasi nzuri ambayo ni vigumu sana kwa yule atakayeufuata barabara kuingiza matabaka haya ambayo hatima yake ni uadui, chuki za kila namna na hatimaye mauaji ya kinyama.
Hebu na tuangalie Qur'an inatuambia nini juu ya matabaka haya: Kwanza, Mwenyezi Mungu ameanza kwa kututanabaisha kuwa wanaadamu wote asili yetu ni moja na tumetokana na nafsi moja.
"Enyi watu! Mcheni Mola wenu ambaye amekuumbeni katika nafsi (asili) moja. Na akamuumba mkewe katika nafsi ile ile. Na akaeneza wanaume wengi na wanawake kutoka katika wawili hao..." (4:1)
Hapa Mwenyezi Mungu anatufahamisha kuwa baada ya Adam (as) kuumbwa kisha akaumbwa mkewe ambaye ni Hawwa (a.s.) ndipo tukaenea wanaume kwa wanawake wengi duniani kutoka katika wawili hao.
Pia katika Qur'an 49:13 Allah (s.w.) anatufahamisha:
"Enyi watu! Kwa hakika tumekuumbeni (nyote) kwa (yule) mwanaume (mmoja, Adamu) na yule yule) mwanamke (mmoja Hawaa). 
Na tumekufanyeni mataifa na makabila (mbalimbali) ili mjuane (tu basi, siyo mkejeliane). Hakika aheshimiwaye sana miongoni mwenu mbele ya Mwenyezi Mungu ni yule ambaye mcha Mungu zaidi katika nyinyi. Kwa yakini Mwenyezi Mungu ni Mjuzi, Mwenye habari (za mambo yote)". (49:13).
Kumbe Mwenyezi Mungu baada ya kutuumba kutokana na nafsi moja, bado alitugawa katika mataifa na makabila tofauti tofauti, lakini si kwa lingine bali ili tuweze kujuana.
Hebu na turejee katika Hadithi ya Mtume (s.a.w.) iliyosimuliwa na Abi Nadhrah, kwamba alimsimulia mtu aliyesikia khutuba ya Mtume (s.a.w.) aliyoitoa katikati ya siku za Tashriq akisema:
"Sikilizeni, hakika Mola wenu ni mmoja na hakika baba yenu ni mmoja. Hakuna ubora kwa Mwarabu kwa asiyekuwa Mwarabu wala hakuna ubora wa mwekundu kwa mweusi wala mweusi ju ya mwekundu. Isipokuwa kwa kumcha Mwenyezi Mungu.
Kisha Mtume (s.a.w.) akauliza nimefikisha ujumbe huu? Maswahaba wakajibu amefikisha mjumbe wa Mwenyezi Mungu".
Pia imesimuliwa toka kwa Ibn Umar (r.a.) kuwa Mtume (s.a.w.) aliwahutubia watu siku ya Fathu Makka akasema:
"Enyi watu! Hakika Mwenyezi Mungu amekutakaseni kutokana na uchafu wa ukabila na kujifakharisha kwa mababa zao. Watu wako wa namna mbili, wa kwanza ni mtu mwema Mcha Mungu na wa pili ni muovu aliyedhalili kwa Mwenyezi Mungu. Na watu wote ni watoto wa Adamui na Mwenyezi Mungu amemuumba Adam kutokana na udongo". (Tirmidh)
Pia Hadithi hii imo katika sahihi Sunnah Tirmidh ya Albaan Vol. 3 hadithi ya 2608.
Kwa hiyo utaona kuwa Uislamu ulikuja kuvunja ukabila na kuondoa utabaka.
Historia ya Uislamu inatuonesha kuwa Mtume wa Allah (s.w.) alimpa Usama uongozi wa jeshi kwenda mpakani mwa Sham kupambana na Warumi. Usama alikuwa mtu mweusi akapewa jeshi ambalo limejaa Waarabu mfano Abubakar ni miongoni mwa waliokuwa ndani ya jeshi hilo.
Ipo mifano mingi sana, mfano Sayidina Bilal ambaye alikuwa Muadhini wa Msikiti wa Mtume (s.a.w.) alikuwa mweusi.
Kwa hiyo kinachoangaliwa katika Uislamu ni uwezo wa kufanya kazi inayotakiwa. 
Kama ni Uimamu au Uamiri au uangalizi wa shughuli yoyote ile inayohusu Uislamu sharti mhusika awe na ujuzi wa yakini juu ya kazi hiyo, ukabila, utaifa na uzawa havitaangaliwa.
Kwa misingi hiyo ndiyo maana Allah (s.w.) akatuunganisha pamoja kwa kutuita ndugu. Soma Qur'an sura ya 49 aya ya 10. Siyo hiyo tu tunaambiwa tupatanishane pale itakapotokea hitilafu baina yetu kisha tumche Mwenyezi Mungu mwingi wa Hekima.
Ndiyo maana Mtume (s.a.w.) kwa kuzingatia hili akasema:
"Mfano wa waumini katika kupendana kwao na kuoneana kwao huruma na kusaidiana kwao ni mfano wa kiwiliwili. Kinapopatwa na maradhi sehemu moja basi mwili wote hukesha kwa maumivu na machovu". (Bukhari na Muslim)
Ninamalizia kwa kuwakumbusha Waislamu wote kwamba tutazame mifano michache ya hapa ulimwenguni juu ya wanaadamu ambao wamethubutu kuweka ukabila mbele zaidi ya utu. 
Matokeo yake ni nini? Sina haja ya kutoa mifano ni nchi gani au ni jimbo gani hapa duniani lenye mgogoro mkubwa wa kijamii unaotokana na ukabila na utabaka.
Lakini ikumbukwe kwamba maadui wa Uislamu waliutumia ukabila na wanaendelea kuutumia ili kuhakikisha Uislamu unaangamizwa kabisa. Angalia maneno ya Mwenyezi Mungu ndani ya Qur'an 63:7-8. 
Na Hashim Rusaganya

No comments:

Post a Comment

Twitter Bird Gadget