Friday, April 20, 2012

Mahari katika Uislamu


Watu wengi huifanya mahari kama ni thamani ya mwanamke na wanadhania kwamba kuighalisha ni nembo ya utukufu wa familia yake. 
Ni kwa ajili/sababu hiyo basi, wanapita kiasi katika kiwango cha mahari na wanaighalisha katika kuifanya kubwa na nyingi ili kuonyesha thamani ya binti/muolewa. 
Na kuonyesha utukufu wa daraja/cheo cha familia yake na kujifakharisha kwa mabinti/wanawake wenzake katika shughuli ya harusi yake na samani za nyumba yake. 
Imetoka kabisa akilini mwa watu hawa, kwamba katu mahari si nembo ya kuonyesha utukufu/thamani au nafasi ya aila (familia) au ukoo fulani mbele ya jamii. 
Kama ambavyo si nyenzo/zana ya kumuandaa muolewa tayari kwa ndoa, bali kamwe si chombo cha kuipambia nyumba ya bi. Harusi mtarajiwa. 
Hakika si vinginevyo, hayo mahari ni alama ionyeshayo ukweli wa matashi na dhamira ya kutaka ndoa kwa upande wa mwanaume. Na kwa upande mwingine ni atwiya (kipawa) kwa ajili ya kumtukuza mwanamke na kuipendezeshea nafsi yake katika ujenzi wa maisha matukufu ya ndoa.
Si hayo tu, pia yako mbali mno na akili za watu hawa, mafisidiko ya kijamii yanayo tokana na jambo hili lichukiwalo, lililo mbali kabisa na ukweli. 
Kama yalivyo ghibu akilini na fikrani mwao, madhara yanayo isibu jamii kwa ujumla. 
Na huyo mwanaume mshindwa kuoa na mwanamke asiye oleka kutokana na ughali wa mahari, kwa ukhusia. Hali kadhalika, haimo akilini mwa watu hawa, kwamba wao wanaikhalifu Suna ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie. 
Kwa kupita/kuifuata kwao njia isiyo ya baraka, baraka ambazo zinasababishwa na wepesi na uchache wa mahari, kama alivyo libainisha hilo Bwana Mtume.
Ama tukiyaangalia hayo maharibiko ya kijamii yanayo sababishwa na ughali wa mahari, ni mengi kathiri. 
Miongoni mwake, ni kwamba ughali wa mahari ni kikwazo kinacho wakwaza vijana kuoa, hasa hasa wale walio mafukara miongoni mwao. Hili la kushindwa kuoa huwapelekea kutokuwa na hiari ila kufuata njia mbaya na chafu ya shetani. 
Na kujikuta tayari wamesha tumbukia katika tendo vunda la zinaa aliyo iharimisha Allah. Tendo linalo wageuzia wema (ndoa) kuwa fisadi/uovu (zinaa), utulivu kuwa mpapariko wa dhamira. 
Natija ya tendo ovu hilo, ni kuchafuka heshima/hadhi ya familia husika, kupotea kwa nasabu, kukithiri kwa watoto wa mitaani sanjari na kuenea kwa maradhi mabaya hilikishi.
Lau vijana hawa walio tumbukia kwenye wimbi la zinaa, wangeli kuwa na wake wanao wakwasia na uchafu huo. Basi hapana hata chembe ya shaka, kwamba wangeli zihifadhi hulka na silka zao sanjari na kuilinda dini yao. 
Na wangeli idhaminia jamii yao kusalimika na madhambi na athari mbaya ya tendo baya la zinaa.
Ama maharibiko yanayo msibu mwanamke mwenyewe yakiwa ni natija ya ughalishwaji wa mahari, inatosha tu kutaja kwamba: Huenda wanawake wengi wakaachwa waseja, walio nyimwa/kosa kile wakihitajiacho kwa mujibu wa maumbile yao na ambacho hawana njia ya kujikwasia nacho, tena kinapondokewa na nafsi zao.
Na wataendelea kuhisi pengo linalo wakosesha usingizi na hivyo kutamani mno kupata mahala patakapo watatulia matatizo yao hayo. 
Mahala ambapo wataihisi neema ya utulivu na ushwari wanayo ikosa kwa sababu tu ya wazazi wao kutaka mahari yanayo wahemeza wengi wanao jitokeza kuwaposa. 
Hayo ndio yanayo wapata pale watakapo kuwa hawakujitokeza majiani na kuleta fitna na kuifisidi jamii yao. 
Ama wakishindwa na maumbile wakaamua kujitosa majiani kama tunavyo ona leo, basi madhara yake huwa ni makubwa mno na enevu kama ishuhudiwavyo leo ulimwenguni kote.
Ama kule kuikhalifu kwao Suna ya Mtume, basi hebu na tuyasikilize kwa mazingatio, haya yasemwayo na Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie:
Imepokewa kutoka kwa Bi. Aysha-Allah amuwiye radhi-amesema: Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Hakika ndoa yenye baraka kushinda ndoa zote, ni ile nyepesi/chache yao mno (hizo ndoa) kwa mahari”. Ahmad [6/82]-Allah amrehemu.
Imepokewa kutoka kwa Sayyidna Umar-Allah amuwiye radhi-amesema-Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Bora ya ndoa ni ile iliyo nyepesi mno”. Abu Daawoud [2117] & Al-Haakim-Allah awarehemu.
Chini ya kivuli cha hadithi hizi, utaona kwamba hakuna baraka wala kheri, pale mahari yatakapo kuwa biashara ya kutafutia faida. Na yatakapo kuwa chombo cha kutafutia malimbikizo na kufakharishana baina ya wanajamii.
Imepokewa kutoka kwa Anas Bin Maalik-Allah amuwiye radhi-kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-aliona athari ya rangi kwenye nguo ya Abdurahman Bin Auf-Allah amuwiye radhi. 
Akauliza: “Ni nini hiki?” Akajibu (Abdurahman): Nimemuoa mwanamke kwa (mahari ya thamani ya) dhahabu ya uzani (uzito) wa kokwa ya tende. (Mtume) akasema: “Allah akubarikie, fanya lima (karamu) la harusi japo kwa (kuchinja) mbuzi”. Bukhaariy [4860] & Muslim [1427]-Allah awarehemu.
Angalia na ufahamu ewe ndugu mwema, Mtume wa Allah anamuombea swahaba wake huyu kupata baraka (kheri nyingi) katika ndoa hii ambayo mahari yake haikuwa ila ni thamani ya dhahabu yenye uzito wa kokwa ya tende. 
Fikiri! Basi ni lipi fungu la hawa waghalishaji mahari katika baraka hizi?!
Imepokewa kutoka kwa Abul-Aujaa-Allah amuwiye radhi-amesema: Nilimsikia Umar Bin Al-Khatwab-Allah amuwiye radhi-akisema: “Msiyafanye ghali mno mahari ya wanawake, kwani hakika hayo mahari yangeli kuwa ni chombo cha utukufu Duniani au uchaMungu Akhera. Basi Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-ndiye angeli kuwa mbora wenu kwa hayo (mahari). Lakini hakupata Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-kumpa mahari yeyote katika wake zake, wala yeyote katika binti zake, hakupewa mahari zaidi ya wakia kumi na mbili za dhahabu [28.349g)”. Bukhaariy, Muslim, Tirmidhiy, Nasaai & Abu Daawoud-Allah awarehemu.
Ufupi wa maelezo yote haya, ni kwamba ughali wa mahari ni jambo chukivu (MAKURUHU) katika Sharia. 
Na kwamba wepesi/uchache katika mahari ni jambo pendelewa (MANDUUBU) na ni sababu/chanzo cha baraka kwa wanandoa na jamii kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment

Twitter Bird Gadget