Kila siku ya maisha binaadamu ana jambo na nafsi yake. Ndio anayofikiri nayo ndio anayopanga nayo, ndio mshauri wake wa kila jambo- zuri na baya, dhaifu na imara. Ndie mwandani wake mkubwa kuliko kitu chengine chochote. Nafsi hawezi kuikimbia kwa sababu ni sehemu yake. Ni yeye mwenyewe ndie nafsi yake. Ni sehemu iliyokaa ndani ya kiwiliwili chake na kwa kuwa imemganda, basi hana budi nayo kama asivyobudi na vitu vingi vyengine. Na kila nafsi ina chapa ya mtu mmoja na haifanani kabisa na nyengine kama zilivyo alama za vidole au viini tete vya wanaadamu. Kwa hivyo kila nafsi ina mtizamo, fikra na misimamo yake ambayo itakuwa imejengwa kutokana na ilivyoongozwa au ilivyolelewa au inavyodekezwa na mwenye nafsi hiyo. Kila siku ya maisha binaadamu yupo na nafsi yake.
Anakwenda nayo na anarudi nayo. Ina muongoza au inampotosha kutegemea vipi ana uhusiano nayo au uhusianao wake nayo. Inategemea ameitia mbolea gani na ameinyunyuzia maji kiasi gani ili impe matunda mazuri. Kama ameikhini mbolea na maji, hawezi kutarajia matunda mazuri, maana kila kilichokhiniwa hakiwezi kuwa na imani na ikikosekana imani njia njema haielekezwi kabisa, bali ni njia potofu. Hili inapaswa tulizingatie kwa kiasi kikubwa. Nafsi ina nguvu na udhaifu wake. Unaweza kusema kwa kiasi sawa. Ina busara na ujinga wake nayo pia kwa nguvu sawa lakini pia ina kila kitu ambacho mwanadamu anacho lakini si kwa maana ya kuonekana ila kwa njia ya kivuli. Nafsi haikamatwi lakini unaihisi, nafsi huioni lakini inakupa mwanga na nafsi huisikii lakini inakusikia vyema wewe.
Ingawa nafsi ina sifa ya kuwa ni kivuli lakini ina ushawishi wa juu na wa pekee kwa binaadamu. Inaweza kumpenya kila sehemu ya mwili wake, inaweza kumzunguka ndani ya mwili wake na inaweza kujaa na hata kustakimu ndani ya viungo vyake. Kwa mfano nafsi iliyoelekeza na kukubaliwa na mwili wa binaadamu inaweza ikawa inampa amri mwenye nafsi kuwa kila akiona mfuko wa suruali ya binaadamu umetuna basi ajisogeze karibu na mkono wake unyooke na vidole vyake vichomowe kipochi kilichomo ndani ya mfuko huo. Au nafsi iliyo elekeza kuwa macho ya binaadamu yanyanyuke kumtizama mwanamke aliyepita mbele yake basi macho hayo hayawezi kabisa kujizuia mpaka yamtizame mwanamke huyo kutoka utosi mpaka kwenye unyayo hata iwapo kitendo hicho kitamhatarisha pengine kwa kukosewa na gari au hata kuadhirika tu kwa mkodoleo huo wake.
Au nitoe mfano mwengine ambao utasaidia kuleta ufahamu wa jinsi tunavyoishi na fasi zetu tukijifanya hatuna maamuzi ilhali ukweli ni kuwa nafsi ni nyenyekevu ikiwa mwenye nafsi atakubali kuwa mnyekekevu maana nafsi penye uimara haiwezi kukinza amri.
Mfano wenyewe ni wa binaadamu kutaka kujua yasemwayo na wengine au tuseme kwa uwazi sikio la umbea. Mara nyingi tunajidai kusema kuwa jicho halina pazia na kuwa pia masikio hayana chujio, lakini hiyo si kweli kabisa. Basi mimi naamini kama nafsi yako itakuwa imara na wawepo watu chini yako wana mazungumzo yao, na kama wewe hutaki kuyasikia basi hutayasikia.
Utakuwa na uwezo kuihamisha akili yako sehemu nyengine na wale walio mbele yako watakuwa ni kivuli tu na wasemacho ni upepo tu ndani ya masikio yako hata kama wako chini ya ubavu wako.
Hebu jiulize hivi mara ngapii ulikuwa ushakaribia kufanya kitendo kiovu, ushakaribia kabisa lakini ukaamua kutokifanya? Uamuzi kama ndio kuiweza nafsi, kuipinda ikatae kutenda vitendo viovu.
Mara ngapi umewahi kujiuliza unatoka na nia kabisa ya kwenda kutoa msaada kwa mtu lakini unafika njiani unabadilisha mawazo kwa kutokwenda au kupunguza msaada ambao ulikusudia kuutoa?
Huko pia ni kuikubalia nafsi yako ikupeleke kusiko maana nia yako kwa sababu ya kuikubalia nafsi yako ikutoe kwenye barabara ya wema na ihsani ambayo ulikuwa umeshaielekeza.
Kwa hivyo wanaadamu kila siku ya Mungu tunapata mitihani na nafsi zetu. Nafsi zetu zinatupa majaribu makubwa na madogo, ya kutujenga duniani na ya kutuangamiza akhera, Nafasi haina kizuizi katika majaribu hayo.
Wakati tunatakiwa tuzipende nafsi zetu na tuzisikilize kwa mambo ya maana na ya msingi basi pia tuzikatalie kwa mambo yasio na maana na ambayo si ya msingi ingawa tutakuwa tunaiudhi nafsi yetu.
Lakini nafsi haiudhiki kwa kuwa haina hisia iwapo imeelekezwa tokea mwanzo, sawa na nafsi inavyokosa kujua baya au ovu iwapo tokea mwanzo haikuelekezwa kutambua jambo hilo.
Tunatakiwa tuzipende sana nafsi zetu. Nafsi zetu tuzipe kinachotaka, tuzipeleke zinakopenda na tusisikilizishe kinachopenda kukisikia. Tusizikhini hata kidogo kwa kuwa kukhini ni kudhulumu na dhuluma ni kafara ambayo itakuja kukurudi japo siku moja.
Tule kwa mujibu wa nafsi zetu ila vya halali; tucheze kadri ya nafsi zetu zinavyopenda ila michezo mizuri. Tuende kadri nafsi zetu zinavyotaka tuende lakini safari za halali. Mfumo uwe ni huo.
Ila nafsi zina mtindo mbaya. Mtindo wa mazoea, mtindo wa kutaka zaidi na zaidi kufikia hata kudai na kulazimisha. Ni vyema tukajenga tabia ya kuweka mipaka kwa nafsi zetu. Nafsi zikajua mpaka ni huu na ziada ya hapa sitapewa hata nitoke machozi ya damu.
Nafsi haitochoka kudai na kulazimisha, lakini wakati mwengine inakuwa ni laghai inaomba na kubembeleza. Tusihadaike maana mwisho wa maneno mambo yakiharibika nafsi inaturuka na inasema ilikuwa ni uamuzi wako wewe peke yako na wewe ndio mwenye maamuzi.
Kwa hiyo kwa kiasi leo tumezindua kuwa nafsi ina mengi na haijui kiasi kama haijafunzwa na kuelekezwa. Kila mara inatupasa tuseme na nafsi yetu na kuiambia mitizamo na misimamo yetu maana tusipofanya hivyo kila siku itafanya tena majaribio kwa kujua kuwa binaadamu ni dhaifu kimaumbile.
Katu tusije tukafanya kosa la kuipenda nafsi hadi kufikia kiwango cha kuiendekeza. Tukifikia hapo tujue maharibiko yanaweza kuwa ni makubwa nayo ni ya hapa duniani na hata akhera kama ambavyo tumeshasema.
Mimi sioni kwa nini tushindwe kuzuia kuzipenda nafsi zetu kupita mpaka na kuziendekeza. Kwani ni wazi kila mmoja wetu kwa wakati mmoja au mwengine amewahi kuikatalia nafsi yake kufanya, kusikiliza au kwenda pahala na bila ya mgogoro. Mgogoro utakujaje wakati madhumuni yako ni kutafuta mizania?
Nafsi inataka ipewe sababu na maelezo, hoja na vipimo ili iridhike.Basi mimi na wewe tunaweza kukosa sababu na maelezo au hoja na vipimo ikiwa hatutaki jambo au tunataka kufanya jambo?
Najua tunaweza na tutasimama kuiambia nafsi yetu kuwa hili la sitakuendekeza. Maana kukuendekeza ni kuharibikiwa na kuharibikiwa wewe si jambo ambalo utalikubali hata kidogo
Bado hujachelewa kujifunza kusema na nafsi yako. Hakuna kuchelewa katika kujizuia kufanya mabaya au kwenda njia mbovu. Kama ulikuwa ukiipenda nafsi yako na hata kufikia kuiendekeza basi fanya dhamira na tengeneza azimio kuwa hapo ulipofika basi na sasa unataka kuongoza njia nyengine. Tafuta muda wa faragha, kaa peke yako na nafsi yako na sema nayo. Ikamate sikio mpaka ikusikie kuwa sasa unataka kuwa mtu mpya na nafsi yako ibadilike pamoja na wewe. Inawezekana kabisa ukiweka nia, na Wapemba wamesema zamani kuwa Jambo Nia...
No comments:
Post a Comment