Wednesday, May 2, 2012

Kisa cha kusilimu kwa muimbaji maarufu (Cat Stevens)

Kisa cha kusilimu kwa muimbaji maarufu (Cat Stevens) 
Akizungumza na Al Bayan, gazeti litolewalo kila siku huko Dubai, mlinganiaji maarufu kutoka Uingereza – (Cat Stevens) aliyejibadilisha jina lake na kujiita Yusuf Islam alisema:

“Mashindano ya ulimwengu ya kusoma Qurani yanayofanyika kila mwaka mjini Dubai ni zawadi adhimu sana kwa Waislamu ulimwenguni yenye kuwaongoza katika kukihifadhi kitabu cha Mwenyezi Mungu kilichobeba miujiza mingi iliyokwisha dhihiri kwa Waislamu na kwa wasiokuwa waislamu.”

Akizungumza juu ya sababu za kusilimu kwake Yusuf Islam alisema kuwa zipo sababu nyingi sana zilizomfanya asilimu. Alihadithia namna gani alivyokuwa karibu na kuzama baharini jambo lililomfanya baada ya hapo aanze kuifanya kazi kubwa ya utafiti na ulinganishaji wa dini na hatimaye kusilimu.

Alizungumza pia juu ya sababu zilizomfanya avutiwe na dini ya Kiislamu ambayo hivi sasa anailingania kwa nguvu na kwa uwezo wake wote, na pia juu ya sababu zilizomfanya awe radhi kuacha shughuli zake za uimbaji zilizokuwa zikimletea utajiri mkubwa na umashuhuri hapa duniani na badala yake akajishughulisha na kazi itakayompatia radhi za Mola wake Subhanahu wa Taala.

Yusuf alisema pia:
“Nilizaliwa katika ukoo wa kidini wenye kufuata mafundisho ya kikristo kwa ukamilifu, jambo lililosababisha kupelekwa katika shule ya kiseminari (missionary school) yenye kufuata madhehebu ya kikatoliki huko London tokea utotoni mwangu na kusomeshwa na mapadri wasiopenda kujadili mambo ya dini wala kuulizwa masuali mengi. Hata hivyo nilikuwa nikielewa vyema kuwa yapo mambo mengi katika dini yangu yasiyokuwa sahihi, lakini sikuwa na la kufanya kwa sababu walimu wangu hawakupenda kuulizwa masuali mengi.”

Mwanzo wa shaka
Niliweza kugundua baadaye kuwa wengi kati ya wale niliosoma nao katika shule za kiseminari waliokuwa daima wakijidai kuwa wanaamini kuwepo kwa siku ya Kiama na Pepo na Moto, lakini mara baada ya kujiunga na shule za kisekula (secular) huanza kuitilia shaka imani yao hiyo, na hii inatokana na sababu za upungufu wa imani katika mambo ya ghaibu.

Shaka ilianza kuingia moyoni mwangu, na hapo ndipo nilipoanza kuingia katika mapambano makubwa na nafsi yangu. Nikawa sina budi kulifikia lengo langu kwa sababu jamii yetu haiwahurumii wasio na uwezo.

Wakati ule mambo ya starehe na anasa za kila aina yalienea kwa nguvu sana. Vilabu vya usiku ‘night clubs’, viwanja vya starehe na vya michezo pamoja na muziki, vyote hivi vilinivutia sana hata nikaamua na mimi pia kujiunga na ulimwengu huo niliokuwa nikiuona ndani ya sinema za Holywood. Wanawake, utajiri, magari na kila anachoweza kukitamani kijana wa kizungu kama mimi vilikuwa vimeenea.

Nikaanza kuwa mtumwa wa matamanio ya nafsi yangu, na hii ndiyo hali aliyokuwa nayo kila mzungu wakati ule. Alikuwa mtumwa wa matamanio ya nafsi yake.

Nikagundua kuwa ili kuyafikia matamanio hayo nilihitajia mambo machache sana kama yale waliyohitajia waimbaji wa kikundi cha ‘Beetles’, nayo ni kubeba gita ‘guitar’, kuanza kutunga nyimbo na kuziimba. Hilo kwangu lilikuwa ni jambo jepesi sana. Kwa njia hiyo nikaingia katika ulimwengu huu na kuanza kujitangaza katika mashirika mpaka nikafanikiwa kupata shirika lililokubali kuninunua. Wakaniwekea sharti la kulibadilisha jina langu kwa sababu jina la mwanzo lilikuwa gumu na geni, na watu wa Uingereza wakati ule hawakuwa wakiwapenda wageni.

Siri ya kulichagua jina langu
Nyimbo yangu ya mwanzo niliyoimba niliiba muziki wake kutoka kwa mtungaji Muislamu aitwae Yusuf Latif. Na pia sura ya mwanzo iliyoniingia moyoni mwangu ni Surat Yusuf.

Nilichagua jila la Cat Stevens kwa sababu naelewa kuwa Waingereza wanapenda sana paka na wanapoteza pesa nyingi sana katika kuwalisha na kuwatunza. Nikajisemea moyoni mwangu: ‘Labda watanipenda kwa jina hili.’

Nikaianza safari yangu katika ulimwengu wa muziki kwa nyimbo inayoitwa; ‘Nampenda mbwa wangu,’ na kwa mshangao mkubwa nyimbo hii ilipata mafanikio makubwa. Kuanzia hapo ndoto zangu zikaanza kuwa kweli na jina langu likawa midomoni mwa watu wote katika ulimwengu wa watu mashuhuri, na watu wengi wakawa wanatamani angalau kuzungumza na mimi au kupata saini yangu katika autograph zao.

Lakini umashuhuri una thamani yake pia, na maisha ya starehe bila ya muongozo hayawezi kuendelea milele. Nikapata maradhi mabaya, na wakati huo nikajikuta ghafla nimo kitandani mbali kabisa na rafiki zangu na mbali na umaarufu na kupigwa mapicha. Na hapo ndipo nilipoanza kuifikiria nafsi yangu na maisha yangu na hali niliyokuwa nayo.

Safari ya kuutafuta ukweli
Kutokana na hali ya kukata tamaa niliyokuwa nayo pamoja na upotofu, nikaamua kuanza kuzidurusu dini mbali mbali. Nikaanza kwa kusoma juu ya dini za upande wa Mashariki ya dunia kama vile ‘Budhism’ wenye kumuabudu Budha, na nikawa nasoma vitabu vinavyoelezea falsafa yake mpaka siku ile nilipokigundua kitabu kinachoitwa ‘Njia ya siri’, na kitabu hicho kilikuwa kikieleza kuwa; mwanadamu hawezi kukinai mpaka pale atakapokumbana na ajali yake isiyokimbilika..

Lazima nikiri hapa kuwa kitabu hiki kilinipa msituo mkubwa kwani mimi nilikuwa nikiutafuta ukweli pamoja na kutaka kuyajua yale nitakayokutana nayo baada ya kufa kwangu. Lakini sijapata ndani ya vitabu hivyo isipokuwa namna ya kutumia muhadarati kwa ajili ya kunisahaulisha mapambano yaliyomo ndani ya nafsi yangu, na kinyume cha hayo hali yangu ilizidi kuharibika na kuwa mbaya sana.

Nikaanza kutunga nyimbo zenye kueleza juu ya dhiki zangu na kuutafuta kwangu ukweli. Safari hii nikafanikiwa sana hasa katika nchi ya Amerika. Umashuhuri wangu ukarudi tena na kamera zikaanza kunielekea na kunifuata kila niendapo. Lakini mafanikio hayo hayakuweza kunipoza moyo wangu na kuniondolea dhiki na maumivu yangu, bali yaliniongezea nguvu ya kuutafuta ukweli juu ya dunia hii.


Kukutana kwangu na Uislamu kwa mara ya mwanzo
Naikumbuka vizuri siku ile nilipoingia ndani ya duka la vitabu vya falsafa na dini. Juu ya mojawapo ya rafu zake kilikuwepo kitabu kinachozungumzia Uislamu. Sikutaka kukinunua kwa sababu baba yangu siku zote alikuwa akinihadithia juu ya ubaya wa Waislamu wa Kituruki.

Kwa ajili hiyo nikaendelea kusoma vitabu vya falsafa mbali mbali lakini sijafuata dini yoyote ile juu ya kuwa niligeuka kuwa mlaji wa mboga mboga na matunda tu (vegetarian) kama ilivyoandikwa katika baadhi ya vitabu vya dini za Mashariki. Nikajishughulisha kujifunza elimu ya kupiga ramli kwa njia ya nyota ili niweze kuujuwa mustakbali wangu, lakini yote hayo hayakunizidishia isipokuwa tabu na dhiki.

Maisha yangu yakaendelea kuwa ya kawaida yenye kuchosha, kwani wakati mwingine huwa mbele ya maelfu ya wapenzi wangu katika mji wa Dallas na mara nyingine hukaa peke yangu huku nikifikiri juu ya nafsi yangu pamoja na yale niliyo ndani yake.

Hatua ya mwanzo kuelekea kwa Mwenyezi Mungu
Siku moja nilipokuwa nikiogelea kandokando ya mojawapo ya bahari za California, nilikwenda mbali na nchi kavu, na wala sikutanabahi kuwa niko peke yangu mpaka pale nilipoamua kurudi nchi kavu. Nilijikuta bila kujihisi kuwa nimekwishaingia ndani ya mkondo wenye nguvu na hapana wa kunisaidia. Nilipata tabu sana. Nikaanza kuogelea kwa nguvu zangu zote ili niyaokoe maisha yangu, na kila nilipojaribu kupambana na mkondo uliokuwa ukinivuta nilitaabika zaidi na hapo ndipo nilipohisi kuwa sitoweza kuokoka.

Nikaanza kuyafikiria mauti na kutambua kuwa hapana atakayeweza kuniokoa isipokuwa Allah. Nikaanza kupiga kelele; ‘Nisaidie ewe Allah na ukinisaidia nitakuwa mja wako mwema na kuitumikia dini yako ya haki.’

Nilikuwa nikielewa kuwa Mwenyezi Mungu anayo dini ya haki, lakini sikuwa nikijuwa kuwa dini hiyo ni Islam. Na kwa hakika nilihisi kama kwamba wimbi hafifu lilinibeba na kunisukuma bila ya kutumia nguvu zozote na punde nikajikuta nimetupwa ukingoni mwa bahari.

Na baada ya kutupwa na wimbi hilo na Mwenyezi Mungu kuniokowa sikuisahau ahadi niliyoitowa, nikaanza kuutafuta tena ukweli utakaonipeleka katika dini ya haki.

Kusilimu
Nikajikuta nimejifunga na ahadi ambayo sikuweza kujuwa nitaitekeleza namna gani, na kama kawaida yetu sisi wanadamu husahau ahadi zetu na kuendelea na maisha, lakini Allah hasahau.

Hazikupita siku nyingi ikanifikia jawabu la suali langu kutoka mahali nisipopategemea kabisa.

Ndugu yangu aliyekuwa safarini Jerusalem aliona baadhi ya misikiti na alikutana na Waislamu. Akaanza kujiuliza juu ya dini hii na juu ya Waislamu hawa wasiokuwa maadui zetu wa Kituruki tunaowaogopa. Alipoingia ndani ya mojawapo ya msikiti hiyo, alipata utulivu mkubwa asiowahi kuupata maishani mwake. Na kwa vile anaielewa juhudi yangu ya kuitafuta dini ya kweli akaninunulia Qurani kama zawadi yangu na kuniletea.

Ndani ya Qurani nikapata majibu ya masuali yangu yote yaliyokuwa yakinitatiza na kunizungusha kichwa changu. Nikasema moyoni mwangu; ‘Hii ndiyo dini ya haki niliyokuwa nikiitafuta’. Nikenda moja kwa moja mpaka katika Islamic Center ya mjini London katika mwaka 1977 na kusilimu hapo.

Namna Qurani tukufu ilivyoniathiri
Nilipoanza tu kuzisoma aya za Mwenyezi Mungu nikahisi kuwa mwenye maneno haya haiwezekani akawa mwanadamu, bali ni Allah atakayeniokoa na ambaye daima alikuwa pamoja nami bila kuhisi.

Kitabu hiki ambacho nilikuwa nikikisikia tu hapo mwanzo na sijapata kukiona nilianza kukigeuzageuza nikitafuta jina la muandishi wake, lakini sijaona chochote, ndipo nilipotambua kuwa niliyonayo ni maneno ya Mwenyezi Mungu na sheria zake kwa ajili ya watu wote.

Aya ya mwanzo niliyoisoma ilianza kwa kauli isemayo; ‘Alhamdu lillahi rabbil aalamin’, na hapo nilihisi raha na utulivu sikupata kuiona maisha yangu. Na kila nilipoendelea kusoma aya za Qurani nilikuwa nikipata utulivu zaidi. Nilishangazwa nilipoona majina ya mitume yote niliyoijuwa yamo huo. Nuh, Ibrahim na Bwana Yesu.

Pekee ambaye sikuwa nikimjuwa alikuwa Bwana wetu Muhammad.

Siku nilipoisoma Surat Yusuf, na kisa chake kimefanana kisasi kikubwa na kile nilichokisoma ndani ya Biblia. Lakini nilipomaliza kuisoma sura hiyo moyo wangu ukaanza kudunda. Na hapo nikajisemea nafsini mwangu; ‘Hiki ndicho kitabu cha Mwenyezi Mungu bila shaka yoyote ile. Na haya ndiyo ambayo lazima niyafuate.’

Nikatambua kuwa neno ‘Muislamu’ halikuwa na maana ya taifa au rangi ya mtu, bali huo ni ufahamu uliokamilika wenye kuleta unyenyekevu kwa Mwenyezi Mungu Mola wa walimwengu wote.

Na hapa ndipo nilipotambua pia kuwa Nabi Ibrahim (Alayhi ssalaam) alikuwa Muislamu. Na kama tutaichunguza Biblia tutaona pia kuwa Bwana Yesu alikwenda penye jabali takatifu, akatoa viatu vyake, akamsalia Mola wake anayesaliwa na kila mtu ulimwenguni.

Nikatambua pia ndani ya Qurani kuwa Allah ni mmoja hana mwana, na hilo - (Allah kuwa na mwana) ni jambo lisilowezekana kabisa.


Kutoka katika upotovu kuelekea katika uongofu

Na kwa njia hii nikaamua kuwa Muislamu kwa sababu ikiwa kweli nia yangu ilikuwa ni kuitafuta haki, basi kwa nini nisiendelee katika njia hiyo?

Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taala anasema:

“Bila shaka dini (ya haki) mbele ya Mwenyezi Mungu ni Uislamu.”

Aali Imran -19

Na akasema:

“Na anayetaka dini isiyokuwa ya Kiislamu basi haitakubaliwa kwake. Naye Akhera atakuwa katika wenye khasara (kubwa kabisa).

Aali Imran - 85

Na neno Khasara kama tunavyojuwa ni neno baya kabisa katika kamusi la Kimarekani. Nikaamua kuwa sitaki kula khasara.

Nikichunguza malezi niliyokulia nayo niliona kuwa mtu aliyelelewa malezi ya Kimarekani na ya Kiingereza hana budi kubadilisha mwenendo na tabia ili apate mafanikio. Uislamu unatupa njia sahihi ya mafanikio na unatupa muongozo usiopingika katika kila nyanja ya maisha, pamoja na uwezo wa kujirekebisha na kujisahihisha pale mtu anapokosea.

Na wakati ule nilikuwa na hamu kubwa sana ya kutaka kujisahihisha na kujirekebisha na kuyamaliza matatizo yangu. Nikawa namuomba Mwenyezi Mungu aniongoze ili niyaweze maisha yangu haya mepya.

Suluhisho la tatizo langu nililiona ndani ya Qurani, katika kauli ya Mwenyezi Mungu aliposema:

“Mwenyezi Mungu amenunua kwa Waislamu nafsi zao na mali zao ili na yeye awape Pepo.”At Tawba – 111

Na huu ndio uliokuwa mwanzo wa mwamko wa kweli. Kwani sisi viumbe tunaelewa vizuri kuwa mauti yatakuja bila shaka yoyote, na kwamba kila kitu mwisho wake kitarudi kwa Mwenyezi Mungu kisha itakuja siku ya hesabu, au kama Wamarekani wanavyoiita ‘Siku ya Malipo’.
Siku yatakapofunguliwa mafaili. Tutakapoona kila mmoja wetu nini alichojitangulizia kwa Mola wake.

Na hivi ndivyo nilivyoingia katika dini ya Kiislamu katika mwaka 1977 na hapana kinachonishughulisha zaidi kuliko kuutafuta Uislamu wangu (Identification yangu), na kwa hakika niliweza kuifikia njia ya matumaini na amani.

Tujikumbushe nafsi zetu kuwa sisi sote ni wafanya makosa, na shetani siku zote anajaribu kutudanganya kuwa hatuwezi kuifikia njia ya kurudi kwa Mwenyezi Mungu, wakati Mwenyezi Mungu anasema kuwa Yeye anasamehe madhambi yote hata yawe makubwa namna gani. Kwa ajili hiyo nilifurahi sana pale niliposilimu kwa kuwa Mwenyezi Mungu atanisamehe madhambi yangu na madaftari yangu yatakuwa meupe kama siku niliyozaliwa na mama yangu. Kwa ajli hiyo nasema: “Astaghfirullah Al Adhiym.”

Msimamo wa Aila yangu
Niliwaarifu aila yangu mara baada ya kusilimu, na kusema kweli wao hawakushangazwa sana kwa sababu walikuwa wakiniona jinsi gani nilivyokuwa nikijishughulisha sana kusoma Qurani kwa utulivu, na walikuwa wakiniona namna gani katika muda mfupi nilivyogeuka kuwa mtu anayependa kusema kweli na mwingi wa kuomba dua na mwenye kupenda kuwasaidia wasiojiweza na kufuata yote yaliyoamrishwa ndani ya Qurani.

Nilipokuwa nikifanya yote hayo nilikuwa nikiyahisi mbadiliko yaliyokuwa yakitokea ndani ya nafsi yangu.

Hata pale mama yangu anaponituma, nilikuwa nikiinuka haraka sana na kumtumikia. Alhamdulillah wazee wangu wote wawili wamesilimu na kuzitamka shahada mbili kabla ya kufariki kwao.


Msimamo wa Sahibu zangu
Ama sahibu zangu wasionijuwa vizuri, au waliokuwa wakidhani kuwa wananijua vizuri walipata msituko mkubwa sana kwani kabla ya kusilimu nilikuwa mtumishi wao na ghafla nikageuka kuwa mtumishi wa Allah. Nilijaribu kuwasiliana nao na kuendeleza urafiki wetu, lakini mwisho nilitambua kuwa kwa ajili ya dini yangu itanibidi nichukue hatua ya kuachana nao.

Magazeti nayo yakaanza kunihujumu. Nikashangaa kwa nini watu hawakioni kile ninachokiona katika Uislamu.

Sikupata tabu kuacha kuvuta sigara na kunywa pombe na kula riba nk. Kwa sababu nilikuwa nina yakini kuwa ni katika maslahi yangu kuachana na uchafu huo.

Wakati mwingine ninapokuwa katika baraza pamoja na sahibu zangu wasiokuwa Waislamu na wakati wa Sala unapoingia huwaambia:’Sorry,’ kisha huondoka na kwenda kusali bila kuwajulisha sababu ya kuondoka kwangu wasije wakahisi vibaya. Lakini siku moja nikaamua kuwajulisha wote kuwa ninaondoka kwa ajili ya kwenda kusali, na jambo hilo liliwafanya sahibu zangu hao waniheshimu zaidi, na tokea siku hiyo sikupata taabu tena.

Akizungumza juu ya sahibu zake aliofanikiwa kuwasilimisha, Yusuf alisema:

“Sielewi idadi yao. Lakini sioni kuwa mimi ndiye niliyewahidi, bali Mwenyezi Mungu ndiye mwenye kuhidi na Yeye Subhanahu wa Taala ndiye aliyetaka wahidike.”

Akaongeza kusema:

“Siku moja nilipokuwa mjini Edinburg kuhudhuria ufunguzi wa msikiti, alinijia mwanamke mmoja akanieleza huku akilia kuwa anatamani mama yake aingie katika dini ya Kiislamu. Nikampa kaseti za mawaidha na vitabu ili ampe, na hazikupita siku nyingi akanijia mwanamke yule na kunishukuru. Nikamuambia:

“Mshukuru Mwenyezi Mungu, kwa sababu Yeye ndiye aliyetaka.”


Namna bora ya kuwalingania watu katika dini ya Kiislamu

Namna bora ya kuwalingania wasiokuwa Waislamu ni kuanza kwa kuwajulisha mafundisho yaliyomo ndani ya dini zote mbili ikiwa kama njia ya kuingiza mapenzi ya Uislamu ndani ya nyoyo zao. Kisha tuwajulishe juu ya utukufu uliomo ndani ya dini ya Kiislamu na maajabu yake bila ya kwanza kuwajulisha juu ya wajibu wake na maamrisho yake. Baada ya kusilimu tuwajulishe juu ya Sala, na baada ya kuanza kusali tuwajulishe kuwa Mwenyezi Mungu amewafaridhishia Zaka. Hivi hivi hatua baada ya hatua.

Lazime tuwe macho tusije tukafanya makosa waliyofanya wakristo katika maudhui haya. Hili ni jukumu kubwa tulilobebeshwa. Ujumbe wa Mwenyezi Mungu usifikishwe kwa ulimu tu, bali lazima kwanza tuhakikishe kuwa matendo yetu pia ni ya Kiislamu, kisha tuwalinganie watu katika njia ya Mwenyezi Mungu kama alivyosema Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW):

“Wavutieni (kwa kuwapa habari za kufurahisha) na wala msiwachukize (kwa kuwapa habari za kuwaudhi). Wepesisheni msiyafanye magumu .”

Kwa hivyo daawa yetu iwe nyepesi yenye kudhihirika (Sema; Ni Mwenyezi Mungu mmoja tu.)

Tusijaribu kuwafikishia risala yote kwa pamoja.

Kutoka kwa Muadh bin Jabal (RA) amesema: “Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) aliponituma kwenda Yemen aliniambia: “Ewe Muadh! Unakwenda kwa watu walioteremshiwa kitabu (Mayahudi na Manasara), basi uwalinganie (kwanza) katika kushuhudia kuwa hapana Mola isipokuwa Allah na kwamba mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu. Wakeshakutii katika hilo utawajulisha kuwa Mwenyezi Mungu amewafaradhishia Sala tano kila usiku na mchana. Na wakeshakutii katika hilo utawajulisha kuwa Mwenyezi Mungu amwewafaradhishia Zaka zitakazochukuliwa kutoka kwa matajiri wao na kupewa masikini wao. Na wakeshakutii katika hilo usije ukawalazimisha tena kutoa katika mali zao wanazozipenda sana (muhimu watoe Zaka na kiwango kiwe kinachokubaliana na sheria). Na uigope dua ya aliyedhulumiwa, kwani haina kizuwizi baina yake na baina ya Mwenyezi Mungu (hapana kitakachoweza kuizuwia dua ya aliyedhulumiwa isifike kwa Mwenyezi Mungu).

Kwa hivyo jambo la mwanzo kwa Muislamu anatakiwa awe na khulqa njema, ‘mwenendo mwema’, ‘tabia njema’, mpole, mkarimu, na hizi ni sifa alizokuwa nazo Mtume wetu Muhammad (SAW).

Tunaweza kujadiliana nao kwa mantiki na dalili zilizo wazi kisha wakakubali kuwa sisi tuko katika haki, lakini watakapoondoka na baada ya muda kupita. Muda mchache tu watasahau yote kwa sababu hawakuona kutoka kwetu matendo. Bibi Aisha (RA) alipoulizwa juu ya tabia za Mtume (SAW) alisema:

“Tabia zake zilikuwa Qurani.” Na maana yake ni kuwa alikuwa na Adabu na Tabia zile zilizoamrishwa ndani ya Qurani. Alikuwa akifuata maamrisho yake kwa ukamilifu na kujiepusha na makatazo yake kwa ukamilifu. Na huu ndio ufunguo. Na pana faida gani mtu kusoma Qurani kwa ulimi tu bila ya kutafakari? Qurani ndiyo ukamilifu wa mafundisho aliyoteremsha Mwenyezi Mungu katika kuzijenga Adabu na Tabia za mwanadamu. Kwa hivyo inatupasa kujipamba nayo na kuifuata katika nyanja zetu zote za maisha, na si kuisoma na kurudia kusoma kila tunapohitimisha bila kutafakari juu ya maamrisho na makatazo yake. Inatupasa tutende mengi na tuseme machache na tukumbuke daima kuwa Allah ndiye Mwenye kumhidi amtakaye katika Uislamu.

Anza kwako
Alipoulizwa juu ya propaganda zinazofanywa na vyombo vya habari dhidi ya Uislamu na sifa ovu wanazozuliwa na namna ya kujikinga nazo Yusuf Islam alisema:

“Ningependa kukubainishia kuwa watu wanao uwezo wa kutofautisha baina ya jema na ovu, na wanao uwezo wa kuzielekeza rai zao. Si watu wote wajinga wanaosadiki kila wanachokisoma au kusikia katika vyombo vya habari. Lakini watakapoona baadhi ya sifa mbaya kutoka kwa Waislamu wenyewe, hapo upo uwezekano wa kuyasadiki yale waliyosoma. Kwa hivyo inatupasa sisi Waisalmu kuilingania dini yetu kwa njia ya kujumuika na watu na kuwasiliana nao. Na habari siku hizi zinaenea kwa haraka sana. Kwa hivyo ukiwa kama ni Muislamu, na ikawa mmojawapo wa watu wa nyumba yako hafuati mafundisho ya dini, basi ni juu yako kumuendea jamaa yako huyo kwanza kabla hujamuendea mtu wa nje ili uhakikishe kuwa watu wako wapo katika amani. Kwa sababu mtu anapokuwa Muislamu asifurahi akadhani kuwa keshaepukana na adhabu. Mwenyezi Mungu anasema:

“Enyi mlioamini! Jiepusheni nafsi zenu na watu wenu na Moto ambao kuni zake ni watu na mawe.”

At Tahriym –6
Sababu za kudhalilishwa kwa Waislamu katika zama hizi

Katika mojawapo ya mihadhara yake chini ya anuani’Qurani njia ya pekee ya kuleta mabadiliko,’ Yusuf Islam alisema:

“Waislamu wanatambua kuwa Qurani ni kitabu kitukufu, lakini hawafaidiki na utukufu wa mafundisho yaliyomo ndani yake pamoja na mawaidha, na hii ndiyo sababu ya udhafu wao. Lazima tufuate mafundisho yaliyomo ndani ya Qurani na Sunnah na hapo ndipo tutakaporudisha zama zetu za ushindi na utukufu wa Uislamu.


Kuacha muziki
Alipoulizwa juu ya uvumi kuwa anataka kurudia muziki Yusuf Islam alisema:

“Habari hizi si za kweli. Nimekwishaacha muziki. Isipokuwa sijaacha utangazaji na uenezaji wa habari za dini. Na hili ni jukumu kubwa la kuieneza dini ya Kiislamu. Naona kuwa huu ni wajibu juu yangu na nitaufanyia kazi kwa nguvu zangu zote”.
Nini hiki?

Akizungumza juu ya mshangao alioupata alipoiona hali ya Waislamu baada ya kusilimu kwake alisema:

“Siku moja nilipokuwa matembezini nchini Misri niliusikia muadhini na wakati wa sala ukaingia lakini nilishangazwa nilipoona watu wakiendelea na shughuli zao bila kujali. Nikajiuliza: ‘Nini hiki?’ watu hawa hawazielewi haki za Mola wao? Lakini nilikuwa nikielewa kuwa Waislamu wa siku hizi si wakamilifu na kwamba Dini ya Islam ndiyo kamilifu.

Nadhani Waislamu wengi wameipoteza njia kwa sababu hawajaifahamu Qurani. Qurani tukufu ndiyo elimu yenye kuongoza kwa mwenye kutaka kuifahamu na kuongoka. Na nadhani Uislamu ni kitu kimoja tu. Nacho ni kujisalimisha mbele ya Mwenyezi Mungu na kumtii Mtume wake (SAW). Na kwangu mimi naona kuwa hiyo ndiyo njia ya pekee ya uhakika itakayonipeleka Peponi.

Naona kuwa Mwenyezi Mungu ameijaalia hazina ya elimu na funguo za maarifa kutapakaa na kuenea kila mahali ulimwenguni. Na ni juu ya Waislamu kuungana wote kwa pamoja ili waweze kuifahamu vizuri dini yao, kwani wote wanaamini kuwa Mwenyezi Mungu ni mmoja na Qurani na Muhammad (SAW) kuwa ni Mtume wa Mwenyezi Mungu.

Kisha baada ya hapo kila mtu ana uhuru wake, kwa sababu kila nafsi itavuna kilichopanda.

Unafanya shughuli gani wakati huu?
Wakati huu mimi ninajishughulisha na kuilingania dini ya Mwenyezi Mungu kwa sababu Yeye ndiye mwenye kuniruzuku na ndiye aliyenisahilishia mambo yangu yote. Ninajaribu kwa uwezo wangu na nguvu zangu zote niwe sababu ya kuisimamisha dini hii hapa Uingereza, na dini ya Kiislamu inapata nguvu kila siku.

Ninajifunza lugha ya Kiarabu na lengo langu hasa nataka niweze kuifahamu Qurani. Waislamu wengi wanaweza kuisoma Qurani kwa lugha ya Kiarabu na kwao wao hilo ni tosha kabisa. Ama kwangu mimi naona kuwa Qurani lazima ifahamike maana yake, kwa sababu kila aya ina muongozo ndani yake. Nasikitishwa sana na watu wanaoisoma bila kuyatafakari yaliyomo ndani ya maneno hayo ya Mwenyezi Mungu Subhanahu wa taala na pia nasikitika kuwa Waislamu hawajakiweka kitabu hiki kuwa ni kitu cha mwanzo ndani ya nyoyo zao.
Sababu zinayowafanya watu wa Ulaya na Wamarekani kusilimu kwa wingi

Nadhani lengo la mwanzo kwa mwanadamu analotaka kulifikia kwa kawaida ni kuwa bora katika elimu itakayomletea maendeleo. Elimu za mawasiliano na nyingine mbali mbali. Akishafanikiwa katika hilo huanza kuhisi kuwa bado pana kasoro Fulani, lakini kasoro hiyo haielewi iko wapi. Na kasoro hii ni katika mambo ya kiroho. Na mwanadamu anahitajia yaliyo bora zaidi katika mambo ya kiroho kupita visa na hadithi na mchezo. Anahitajia jambo kubwa na tukufu zaidi. Na kwa ajili hiyo mimi naona kuwa ndani ya Uislamu linapatikana ponyo la kuiondoa dhiki hiyo. Mimi nilipata katika Uislamu yote niliyoyahitajia. Nilipata yale ambayo kabla ya kusilimu kwangu juu ya utajiri, ujana na umaarufu niliokuwa nao sikuweza kuyapata.

Kwa ajili hiyo watu wa nchi za Magharibi wanaitafuta furaha ndani ya mali na ndani ya kitu ‘material’, wakidhani kuwa humo wataipata furaha hiyo. Lakini walichokuwa nacho ni wakati mwingi wanaoupoteza bure, na kwa ajili hiyo maisha yao yanakwenda bila ya mezani. Ndani ya Uislamu wanaipata mezani hiyo kwa sababu Uislamu haufundishi mambo ya kiroho peke yake, bali unafundisha yote mawili (roho na mwili).

Ndani ya dini za Kikristo na Kiyahudi yapo mambo ya kiroho pia. Lakini sisi tunaigia katika karne ya ishirini na moja. Wao wanatafuta mambo ya kisasa kabisa. Programu mpya za computer, magari mepya ya kisasa. Hawataki ujana wao upotee bila ya kuvitumia vyombo vya kisasa. Kwao wao mambo ya kidini hayana umuhimu kuliko mambo ya kidunia. Kwa hivyo wanatafuta dini inayokwenda sambamba na maendeleo ya kisasa. Dini ambayo unaweza kuwa mtu wa dini na wakati huo huo unaweza kuvitumia vyombo vya kisasa.

Kwa ajili hiyo Islam ndiyo dini inayofaa katika wakati wetu huu na mpaka siku ya Kiama. Kwa sababu Muhammad (SAW) amekuja na ujumbe kutoka kwa Mola wake kwa ajili ya wanadamu, na ujumbe huu ni wa mwisho na kwa wanadamu wote.

Vyombo vya habari vya nchi za Magharibi vinajaribu kufahamisha watu makosa ya kisiasa yanayofanywa na viongozi wa Kiislamu. Jambo ambalo nchi za Kiislamu zipo nyuma katika wakati wetu huu. Na hii ni kwa ajili ya kutaka kuwaonesha watu kuwa hapana cha kuvutia katika dini ya Kiislamu. Lakini ndani ya Uislamu mna utajiri mkubwa kupita kila kitu duniani. Mna hazina kubwa katika mafundisho ya Mwenendo na Tabia njema na katika mambo yote ya kilimwengu na katika kila anachokihitajia mwanadamu.


Mafanikio ya nchi za Magharibi
Nadhani kuwa asili ya mafanikio katika nchi za Magharibi ni kuwa wao wanapanga na wanafuata nidhamu maalum. Ulimwengu huu unafanya kazi yake sawa sawa kwa sababu Mwenyezi Mungu ameuwekea nidhamu maalum, na lau kama isingekuwa hivyo mambo yote yangeliharibika.

Na nchi za Magharibi zimefanikiwa kuweka nidhamu katika nchi zao inayowawezesha kuwaletea mafanikio na maendeleo juu ya khitilafu kubwa iliyokuwepo baina yao. Utulivu na amani vinaharakisha maendeleo katika nchi. Lakini bahati mbaya nchi hizi haziwapi fursa nchi za Kiislamu kupata utulivu na amani, jambo linalosababisha kuleta vurugu katika nchi zao na kwa ajili hiyo hatuwezi kupata maendeleo kwa wepesi.

Naamini kuwa yapo makubaliano fulani baina ya nchi za Magharibi kwa ajili ya kutozipa fursa nchi za Kiislamu kupata utulivu na kuwa na uwezo wa kujiendeleza, na kwa ajili hiyo tunazama katika matatizo na zogo lenye kutuzuwia tusijishughulishe na kujiendeleza.

Jambo lingine ni kuwa nchi za Kiislamu hazijiwekei mpango maalum wa kuufuata. Tunapenda kuiga kila kinachotoka nchi za Magharibi na kuiacha kadhia yetu ya asili.

Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) ametufundisha kuwa kama mtu anao mche anataka kuupanda basi aupande hata kama Kiama kinasimama.


Karne ya 21
Karne ya 21 hiyo inaingia na nchi za Kiislamu bado hazina msimamo mmoja. Ni jambo la dharura kwa nchi hizi kuungana na kuwa na msimamo mmoja kwa ajili ya maslahi ya umma. Angalia namna gani Umoja wa Mataifa unavyojiamulia mambo kwa kupendelea upande mmoja kiasi ambapo nchi za Kiislamu hazina uwezo wa kujipatia haki zao.

Kwa hivyo ni katika maslahi ya nchi za Kiislamu kuungana na kuwa na neno lao moja katika umoja huu. Si rahisi kulifikia lengo hilo. Lakini kama utakuwepo mpango wenye muda mrefu na tukaanza hatua baada ya hatua tutalifikia lengo hilo. Pia haitokuwa rahisi kulifikia lengo hilo ikiwa tutaendelea kuitegemea teknolojia ya nchi za Magharibi katika kila nyanja ya maisha yetu. Tunazinunua fikra zao, tunatizama filam zao na kuwafuata katika mengi mengine ya namna hiyo.

Si kwamba kila kinachotoka nchi za Magharibi ni makosa. Lakini; hivyo kweli sisi hatuna uwezo wa kufikiri na kupanga na kuamua, juu ya kuwa tunavyo vile vinavyotuwezesha kufanya hivyo? Hivyo sisi hatuwezi kuwa wavumbuzi. Kwanini basi siku zote tuwe watumiaji tu?

Ukweli ni kuwa lazima tutafute njia za kujiendeleza na kuvumbua. Vitu vingapi tulivyovumbua katika karne hii? Tumeweza kuupa ulimwengu yale tuliyokuwa tukiupa hapo mwanzo?

Je, tumeweza kwa mfano kuendeleza njia za umwagiaji wa maji katika mashamba yetu? Tumeweza kufanya mpango wowote wa kuendeleza taa za barabarani na majumbani au kuvumbua lolote katika mambo ya umeme? Tumeweza kuvumbua njia mpya za kutunza mazao na vitu vyetu?

Mimi naamini kuwa tunayo mengi tunayoweza kutenda katika kuendeleza maisha ya watu ulimwenguni, na jambo hili bila shaka litatuweka mahali petu tunapostahiki kuwa katika ulimwengu huu.

Tunatakiwa tusiwe wenye kujipendelea nafsi zetu tu, bali tushirikiane sote kwa pamoja na kusaidiana katika kulifikia lengo hili.

Mimi naamini kuwa hili linawezekana kabisa Inshaallah. Kwa sababu tunao Waislamu wengi wenye kufanya kazi katika maeneo mbali mbali ya kisayansi na uvumbuzi, lakini tatizo ni kuwa hawajiwekei lengo la mbali. Lazima tujiwekee malengo ya mbali, tusitazame karibu tu. Lengo la mbali linataka subira kwa sababu linachukuwa muda mrefu kulifikia, lakini faida yake ni kubwa zaidi. Katika mfumo huu hapana wataalamu wengi wa Kiislamu wanaojishughulisha.

Karne ijayo ni ya dini ya Islam
Naamini kuwa karne ijayo ni yetu, na naamini pia kuwa mambo hayatokuwa mepesi, juu ya kuelewa vizuri kuwa wakati unakwenda haraka sana. Katika nchi za Magharibi wiki moja inapita kama saa moja tu. Kwa hivyo wakati unakwenda haraka. Sielewi itachukua muda gani, lakini naelewa kuwa vyombo vya mawasiliano ya haraka vitachukua nafasi kubwa katika kuuendeleza ulimwengu au katika kuubomoa. Na kama Waislamu wana nia ya kweli basi mabadiliko yatapatikana haraka sana. Lakini ni juu yetu kupanga na kuyapa maudhui haya umbele ili tuwe na uhakika na kuelewa vizuri wapi tunaelekea.

Uislamu ndiyo dini inayoweza kwenda vizuri na kuzistahamilia dini nyingine. Chukua kwa mfano Madina katika wakati wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW). Ilikuwa dola ya mwanzo iliyokuwa na dini mbali mbali yenye uhuru wa kuabudu. Haya yaliendelea vizuri mpaka ilipotokea khiana na mnaelewa kilichotokea baada ya hapo. Uislamu hautafuti vita wala mapambano, lakini unapolazimishwa kupambana basi unafanya hivyo.

Kuwepo kwa makundi yenye kufuata siasa kali ni matokeo ya kubanwa sana kwa makundi haya mpaka kufikia katika hali hiyo. Lau kama dini ya Kiislamu itapewa haki yake tusingefika kote huko. Mimi sioni kama kadhia hii inafaa kupewa umbele. Kadhia muhimu ni kupatikana kwa amani na utulivu katika Mashariki ya kati. Kwa nini basi tusitafute ufumbuzi wa matatizo sugu tuliyonayo kwa muda mrefu? Ikiwa tutaendelea katika hali hii basi bila shaka matatizo yataendelea.

No comments:

Post a Comment

Twitter Bird Gadget